MAN U WASHANGILIA KIFO CHA GLAZER

No Comments
20140530-055250-21170371.jpg

Man U washangilia kifo cha Glazer

By Israel Saria on May 30, 2014
Washabiki wa Manchester United wamegawanyika baada ya kutangazwa habari za kifo cha mmiliki wa klabu hiyo, Malcolm Glazer kambi moja ikishangilia waziwazi.
Glazer alisababisha sintofahamu Old Trafford alipoinunua klabu hiyo, ambapo washabiki waliandamana kupinga kuuzwa klabu kwa Mmarekani na pia baadhi ya wachezaji wakajifungamanisha na kambi hiyo.
Washabiki walijitokeza kwenye mitandao ya jamii wakionesha kama vile wametua mzigo fulani kwa kifo chake, licha ya kwamba bado umiliki wa Man U unabaki kwa watoto wake sita ambao wamegawana sawa asilimia 90 ya hisa za klabu na nyingine 10 zimewekezwa kwenye Soko la Mitaji la New York.
“Tuna sherehe kubwa leo kutokana na Glazer kufariki dunia, tutakuwa na karamu ya jelly na ice cream kutokana na kifo hicho,” ni maneno ya kawaida kwenye korido za Old Trafford kwa washabiki wanaoichukia familia hiyo kutokana na kununua klabu yao.
Kambi ya pili ni ya washabiki ambao hawalii lakini wanawaasa wenzao kutulia kama waungwana. Wakawalaani wenzao wakisema si jambo la kawaida kwa mtu kufurahia kifo cha mwanadamu mwingine hata kama hawakuwa wakimpenda.
Kambi ya tatu ni ya washabiki ambao wanaonekana kukunjamana nyuso zao wakimlilia Glazer (85)  ambaye daima walikuwa wakimuunga mkono tangu aliponunua klabu 2005 kwa pauni milioni 790, wakisema chini yake palikuwa na mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na ubingwa wa nchi mara tano na mara moja ule wa Ulaya.
Sir Alex Ferguson amekuwa akiwaunga mkono na kuwapinga washabiki waliokuwa wakiwachagiza Glazers, akisema ni watu wazuri ambao hawakuingilia kazi yake. Mwaka 2010 kulikuwa na maandamano na kutolewa kauli chafu dhidi ya mwekezaji huyo na familia yake kwenye dimba la Old Trafford.
Glazer hakupata kutia mguu wake Old Trafford na washabiki wanamkasirikia kwa madai kwamba aliisababishia klabu madeni makubwa yanayofikia pauni milioni 680 huku akichuma faida yeye na familia yake.
Haijajulikana athari za kifo hicho zitakuwa zipi kwa klabu, ikiwa ni miezi 11 tangu Kocha Ferguson aliyeiongoza klabu kwa miaka 26 ang’atuke na miezi kama hiyo tangu kocha aliyemrithi kwa makubaliano na Glazer, David Moyes afukuzwe kazi na chapa ya United kushuka thamani kimataifa.
cdt:tanzaniaspot.com

Dear readers, after reading the Content please ask for advice and to provide constructive feedback Please Write Relevant Comment with Polite Language.Your comments inspired me to continue blogging. Your opinion much more valuable to me. Thank you.