MBWANA SAMATTA HATIHATI KUIKOSA MECHI ZA TAIFA STARS DHIDI YA ZIMBABWE

No Comments
10418977_738351759562105_7960579550010362518_nMbwana Samatta siku alipoumia wakati TP Mazembe ikikabiliana na AS Vita mei 25 mwaka huu.
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania anayeichezea klabu ya TP Mazembe ya DR Congo, Mbwana Ally Samatta yuko hatihati kuichezea timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars katika mchezo wa marudiano kesho kutwa (jumapili) dhidi ya Zimbabwe, mjini Harare, kuwania kupangwa hatua ya makundi kusaka tiketi ya kushiriki kombe la mataifa ya Afrika, AFCON mwakani nchini Morocco.
Taarifa za uhakika ni kwamba Samatta alipata majeruhi ya nyama za paja katika mechi ya ligi ya mabingwa barani Afrika mei 25 mwaka huu dhidi ya wapinzani wao AS Vita mjini Lubumbashi, huku akifunga bao pekee katika ushindi wa TP Mazembe wa bao 1-0. Katika mchezo huo, Samatta alitolewa dakika ya 75 kutokana na majeruhi hayo.
Hata hivyo imeelezwa kuwa shirikisho la soka Tanzania, TFF, baada ya kuambiwa na TP Mazembe kuwa Samatta ni majeruhi, wao walilazimisha kumtumia mchezaji huyo.
Ili kukwepa kuonekana msaliti ameamua kusafiri kwenda Zimbabwe pamoja na Thomas Ulimwengu na kuna uwezekano mkubwa kwa Samatta kukaa kama mtazamaji katika mechi hiyo kwani mpaka sasa hajapona majeruhi hayo.
Meneja wa Mbwana Samatta, Jamal Kisongo amethibitisha taarifa za kuumia kwa nyota huyo tegemeo wa TP Mazembe na kueleza kuwa amelazimika kwenda Zimbabwe ili kutoonekana msaliti.
Mahojiano yalikuwa baina ya mwandishi wa mtandao huu na meneja wa Samatta yamekwenda hivi;
Mwandishi: Jamal Kisongo kuna taarifa za Mbwana Samatta kusumbuliwa na majeruhi ya nyama za paja, vipi kuna ukweli wowote?
Kisongo: Ni kweli! Samatta baada ya mechi ya AS Vita na kufunga bao katika dakika ya 62, dakika ya 75 akawa amepata majeraha ya nyama za paja kujivuta, ikabidi pale pale akatishe kuendelea na mechi. Na toka siku hiyo baada ya mechi ile ya Vita mpaka leo hii hajafanya mazoezi, yaani hayuko katika hali vizuri. Mimi nashangaa, leo nikapata taarifa wakati anaenda Zimbabwe. Mtoto mwenyewe kaniambia anakwenda huko, lakini amelazimishwa na ili asionekane msaliti ameamua kwenda.
Mimi binafsi vitu hivi havinivutii sana, kwasababu wakati mwingine Mbwana anacheza vibaya hapa, lakini anakuwa katika hali ngumu. Mara ya mwisho alipata tatizo la kuzomewa hapa, Mbwana hakucheza mechi kwasababu aliumia Zambia. Kwahiyo amekwenda, lakini mechi hii sidhani kama Mbwana atacheza.
Mwandishi: Mbwana amekueleza nini juu ya mawasiliano yake na TFF juu ya hali yake?
Kisongo: Hapana! Yeye ameniandikia `meseji` kuwa anakwenda katika hali hiyo hiyo na yeye hakutaka kuonesha kuwa anakwepa majukumu ya timu ya taifa. Unajua Mbwana si mtu wa maelezo mengi na alivyonitaka ushauri nilimwambia anatakiwa kutii amri ya viongozi wake kwasababu hata mwalimu wa TP Mazembe mwenyewe baada ya kuona hali hiyo akamwambia wewe nenda tu. Na mimi nikamwambia anatakiwa kutii amri ya TFF, labda wanataka aungane na wenzake ili awatie hamasa, labda uwepo wake utachangia kuongeza hamasa, lakini kama atacheza itakuwa ni kumuumiza na itakuwa vibaya.
Hata ripoti ya daktari inaonesha kuwa huyu kijana ni mdogo na hakugongwa, lakini inaoneakana anatumika sana, kwa maana hiyo uchovu ndio unasababisha majeraha haya.
Mwandishi: Samatta anazungumziaje kuzomewa na mashabiki wa Tanzania?
Kisongo: Yeye anasikitika sana kwasababu tukio hilo limetokea mara moja kipindi ambacho alishindwa kuitumika nchi yake baada ya kuumia nchini Zambia ambako TP Mazembe ilikuwa na mechi. Aliumia vibaya kwahiyo alishindwa kuitumikia timu ya taifa. Hata kule Congo hakupata matibabu, alipokuja hapa Tanzania, ilibidi nimshughulikie na kumpeleka Muhimbili. Lakini bahati Mbaya huwa hakuna ufuatiliaji wa watoto hawa kwa TFF.
Mwandishi: Kwanini Samatta anaumia mara kwa mara?
Kisongo: Unajua sasa hivi wachezaji wengi muhimu wameondoka TP Mazembe. Samatta ni jicho la klabu hiyo kwasasa. Umekuwa akitumika sana. Kwa mfano katika mechi na AS Vita, ilijulikana kuwa Samatta ndio siri ya mafanikio ya Mazembe kwa sasa. Alikabwa kwa nguvu na kuumia. Lakini anasikitika sana kushindwa kulitumikia taifa lake. 
Kutokana na majukumu yake, hakuna sababu ya kumchukua kwenye mashindano kama ya `Challenge`. Wanamuongeza mechi nyingi nzito. Wanatakiwa kumuacha apumzike ili anapokuja kwenye mechi kama hizi za kufuzu basi awe katika kiwango kizuri.
Mwandishi: Ipi kauli yako kwa mashabiki wa Tanzania?
Kisongo: Ninachotaka kusema ni kwamba, huyu mtoto analipenda taifa lake, na watanzania wajue hilo na anaumia sana kutolitumikia kwasasa. Hata kama atalazimika kucheza Zimbabwe, tusitarajie makubwa kutoka kwake kutokana na hali halisi ya afya yake.
Mwandishi: Kisongo asante sana na kazi njema.
Kisongo: Shukurani sana nawe pia!
Chanzo: http://shaffihdauda.com/






Dear readers, after reading the Content please ask for advice and to provide constructive feedback Please Write Relevant Comment with Polite Language.Your comments inspired me to continue blogging. Your opinion much more valuable to me. Thank you.